TAARIFA MPYA ZA USAJILI KUTOKA SIMBA LEO

TAARIFA MPYA ZA USAJILI KUTOKA SIMBA LEO

0

KAMATI ya Usajili ya Simba chini ya Mwenyekiti wake, Zacharia Hanspoppe itakutana wiki hii na benchi la ufundi kujadili jinsi ya kufanya usajili ambao umependekezwa na benchi hilo.

Taarifa ambazo hazina shaka kutoka ndani ya kamati hiyo kuwa tayari wana majina kadhaa ambayo yamependekezwa na benchi la ufundi la kocha Joseph Omog.

Kocha huyo inaelezwa amependekeza asajiliwe kipa mwingine wa maana ambaye si raia wa kigeni ili kuziba nafasi ya Said Mohammed ‘Nduda’ mwenye majeraha ya muda mrefu tangu alipoumia katika maandalizi ya Ligi Kuu Bara visiwani Zanzibar.

Omog alisema kuna uwezekano mkubwa wa Nduda kutocheza mwaka huu na ndio maana amesisitiza kamati hiyo ambayo watakutana nayo wiki hii kukamilisha usajili wa kipa mzawa haraka.

“Tumesajili makipa watatu msimu huu, lakini wamebaki wawili kutokana na mmoja kuwa na majeraha na nafasi hiyo ni muhimu na si jambo zuri kuwa na makipa wawili huku tukiwa na michuano mingi kwani mmoja akipata shida linaweza kuwa tatizo,” kilisema chanzo chetu.

Daktari wa Simba, Yassin Gembe, alisema Nduda bado yupo katika matibabu na anatakiwa kupata muda zaidi wa kutibiwa na kupumzika kutokana na upasuaji wake wa goti uliofanyika India mwezi uliopita.

Naye Omog aliongeza: “Kuhusu baadhi ya wachezaji kutaka kuondoka kwa kuwa wanakaa benchi, hilo ni jambo linalotokea katika timu zote tu.

“Wachezaji waliopo kikosini wote nawahitaji, lakini kama kuna ambaye atataka kuondoka kwa sababu zake binafsi sitaweza kumzuia.”

Source : Mwanaspoti.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY