USAJILI: FAHAMU WACHEZAJI WATATU WANAOTAJWA KUTUA SIMBA DIRISHA DOGO

USAJILI: FAHAMU WACHEZAJI WATATU WANAOTAJWA KUTUA SIMBA DIRISHA DOGO

0

SIMBA inapiga tizi la maana kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam kila siku jioni tayari kwa mechi ya Lipuli itakayopigwa keshokutwa Jumapili Uwanja wa Uhuru na leo Ijumaa itaingia kambini hotelini Sea Scape.

Lakini Kamati ya Usajili imeanza kazi yake baada ya majadiliano marefu kwenye kikao chao na benchi la ufundi. Imeanza mazungumzo na wachezaji watatu wapya mmoja akiwa ni Shasir Nahima kutoka Rayon Sports ya Rwanda anayekuja kuchukua nafasi ya Laudit Mavugo anayepelekwa Gor Mahia ya Kenya kwa mkopo.

Wengine ni Hassan Kabunda wa Mwadui FC ambaye mkataba wake hapo umebakiza miezi sita tu pamoja na kipa wao wa zamani Deogratius Munishi ‘Dida’ ambaye kwa sasa yupo Pretoria University ya Daraja la Kwanza Afrika Kusini.

Habari zinasema Kocha Msaidizi wa Wana Msimbazi hao, Masoud Djuma, ndiye aliyependekeza jina la Shasir baada ya kuangalia mahitaji ya Simba katika wiki kadhaa alizokaa klabuni hapo.

Kwa mujibu wa habari hizo, Simba wamefikia makubaliano ya kumuongeza mchezaji huyo kutokana na mianya waliyoishtukia kwa wachezaji waliopo sasa ambao ni Mganda Emmanuel Okwi aliye fiti kwa kubahatisha huku John Bocco akiwa hatabiriki kutokana na majeruhi yake.

Kuhusu Kabunda, wamepanga kumsajili ili kumpa changamoto Shiza Kichuya ambaye ameonekana kufanya kazi kubwa peke yake, lakini Dida ambaye aliwahi kuichezea Simba kabla ya kujiunga na Yanga, anarudishwa Msimbazi kushika nafasi ya Said Mohammed ‘Nduda’ ambaye ni majeruhi na hawezi kurejea uwanjani mpaka mwakani.

Ingawa Nduda mwenyewe amekuwa akisisitiza Simba wasiwe na hofu atakuwa fiti Januari, Kocha Joseph Omog amewaambia viongozi kuwa anataka kipa mpya mwenye ushindani haraka sana kabla dirisha dogo halijafungwa Desemba 15.

Dida ni miongoni mwa makipa wenye uzoefu nchini ambaye Simba wameona anaweza kumpa changamoto Aishi Manula kwa sasa na kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani.

Habari za ndani zinasema pia kuwa pancha za Method Mwanjali, Shomary Kapombe na Salim Mbonde, zimemtisha Omog ambaye amewaagiza viongozi waangalie uwezekano wa kupata beki mwenye uwezo wa kucheza katikati na pembeni, jambo ambalo nalo pia wanalifanyia kazi kwa siri.
Source : Mwanaspoti

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY