Kwa kujituma zoezini Mwinyi Zahera awanyooshea mikono hawa

Kwa kujituma zoezini Mwinyi Zahera awanyooshea mikono hawa

0

Kwa kujituma zoezini Mwinyi Zahera awanyooshea mikono hawa

KIKOSI cha Yanga kipo mjini Morogoro tangu alhamisi na jana (Juzi) kilifanya mazoezi ya kufa mtu yaliyoambatana na ulinzi mkali katika Uwanja maarufu wa Jamhuri, uliopo mjini humo.

Ipo hivi, Yanga waliondoka jijini Dar es Salaam Alhamisi na Ijumaa walianza mazoezi katika uwanja huo, lakini jana hali ilikuwa tofauti, kwani ulinzi uliongezwa, hakuna shabiki aliyeruhusiwa kuingia.

Mazoezi hayo yalianza saa 2 asubuhi na kufikia tamati saa 4.  Kocha wa timu hiyo, Mwinyi Zahera, aliwahenyesha wachezaji kwa mazoezi maalumu ya kutafuta pumzi ili kuwaweka tayari kwa hatua nyingine aliyosema itakuwa magumu zaidi.

Katika mazoezi hayo, wachezaji walikuwa wakipanda ngazi za uwanja huo na kushuka kwa kasi na pia kutumia muda mwingi kufanya mazoezi ya viungo.

Ndani ya kikosi hicho wachezaji watatu, Said Makapu, Gadiel Michale na Papy Kabamba Tshishimbi ndio waliofunika katika mazoezi hayo, kwa kuzingatia maelekezo ya kocha na pia kufanya vizuri kila walipopewa jaribio.

“Wachezaji hawa ndio waliolianzisha hili zoezi la nguvu na kulifanya kwa mafanikio, nawapongeza na nataka wachezaji wote waige mfano wao,” alisema Kocha Zahera.

Akizungumza nasi baada ya mazoezi hayo, kocha huyo alieleza kufurahishwa na jinsi wachezaji wanavyofuata maelekezo yake kiasi kwamba inampa matumaini ya kufanya vizuri katika michuano itakayokuja mbele yao.

Yanga inatarajia kucheza mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya USM Alger, Agosti 19, jijini Dar es Salaam na baadaye kujiandaa na michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, itakayoanza Agosti 22.

Nahodha wa Yanga, Kelvin Yondani, amewataka wachezaji wenzake kujituma ili kuendelea kuthamini nafasi yao ya kuchezea klabu hiyo kubwa na yenye historia ndefu nchini.

Alisema ana uhakika timu iko vizuri na itafanya vizuri kutokana na jinsi kocha alivyoanza kuinoa na vilevile hamasa anayoiona kutoka kwa wachezaji wenzake.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY