Yanga yafunga dili la Masoud Djuma

Yanga yafunga dili la Masoud Djuma

0

Yanga yafunga dili la Masoud Djuma

KWA takribani wiki nzima sasa, kumekuwa na taarifa za Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, juu ya mpango wake wa kuiacha klabu yake hiyo na kujiunga na mahasimu wao, Yanga, huku habari zake zikipamba vichwa mbalimbali vya magazeti nchini.

Kocha huyo ambaye ni kipenzi cha Wanamsimbazi kutokana na mafanikio aliyoipa timu hiyo tangu ajiunge nayo muda mfupi alipomrithi Joseph Omog, alisababisha sintofahamu miongoni mwa mashabiki wa klabu hiyo juu ya taarifa za kuondoka kwake.

Lakini wiki hii unaweza kusema mjadala huo umefungwa rasmi na sasa kocha huyo ataendelea kuwa mtiifu ndani ya klabu yake ya Simba, huku akisaidia kukinoa kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya kushiriki michuano ya Ligi Kuu inayoendelea hivi sasa.

Kumalizika kwa sakata hilo linalohusishwa na kutoelewana na Kocha Mkuu, Patrick Aussems, kumekuja baada ya kikao cha usuluhishi kilichofanyika kwa ajili ya kuweka mambo sawa baada ya taarifa za kutimka kwa kocha huyo kuenea kila kona.

Licha ya kwamba kikao hicho kilifanyika kwa siri ili kuweka mambo shwari katika klabu hiyo, lakini habari ambazo tumezipata zimesema kwamba, viongozi walitumia busara kuhakikisha makocha hao wanafanya kazi pamoja na pia kuzima jaribio la kwenda Yanga kwa kocha Djuma.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba aliyekuwamo kikaoni, alituambia kwamba, suala hilo kwa sasa limemalizika na kwamba benchi la ufundi limejenga mshikamano na kufanya kazi kwa nia moja.

Kocha huyo anayeheshimu kazi yake na kuipenda anafahamika zaidi nchini Rwanda kama ni mtu asiyependa kuburuzwa, hasa anapokuwa anatetea anachokiamini.

Katika moja ya mambo yaliyomshinda katika klabu ya Rayon Sport ya Rwanda ambayo alikuwa akiinoa ni kuingiliwa majukumu ya kiufundi uwanjani, hali iliyomfanya kukubali kutua Msimbazi akiwa kama msaidizi.

Akiwa Simba aliiwezesha timu hiyo kuweka rekodi ya kufunga mabao mengi katika mechi mbalimbali, rekodi ambayo haijarudi hadi hivi sasa.

Kazi nyingine ambayo kocha huyo anajivunia muda mfupi baada ya kutua Simba ni kufanya mabadiliko ya namba kwa wachezaji, ambapo alimbadilisha Nicolaus Gyan aliyekuwa kama mshambuliaji wa kati na kuwa beki wa pembeni na wakati mwingine akitumiwa kama winga.

Vilevile Jamali Mwambeleko aliyekuwa akicheza beki wa kushoto na kuwa winga wa upande huohuo wa kushoto.

Source : Dimba

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY