Samatta atengewa bilioni 34 England

Samatta atengewa bilioni 34 England

0

Samatta atengewa bilioni 34 England

NYOTA ya nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta, imezidi kung’aa baada ya klabu ya Cardiff inayoshiriki Ligi Kuu nchini England, kuweka mezani Euro 13 sawa na Sh bilioni 34.2 za Kitanzania kumsajili straika huyo.

Taarifa ambazo zimeripotiwa na magazeti mbalimbali nchini England ikiwamo gazeti kongwe la Daily Mail, zinadai kuwa Cardiff wamevutiwa na kasi ya ufungaji aliyonayo Samatta na wanataka kutumia kipindi hiki cha dirisha dogo kumsajili.

Samatta ambaye anakipiga katika klabu ya Genk ya Ubelgiji, amekuwa akiwindwa na timu mbalimbali zinazoshiriki Ligi Kuu mataifa tofauti tofauti ambapo sasa huenda bahati ikamwangukia.

Katika dirisha kubwa la usajili msimu uliopita, Samatta pia alikuwa akiwindwa na timu mbalimbali ikiwamo Levante ya Hispania, Fenerbahce ya Uturuki pamoja na Borussia Dortmund inayoshiriki Ligi Kuu Ujerumani, lakini sasa Cardiff wanataka kumaliza kazi.

Samatta ndiye anayeongoza katika ufungaji Ligi Kuu nchini Ubelgiji akiwa na mabao 15, huku timu yake ya Genk ikishika usukani ikiwa na pointi 48 ikifuatiwa na Club Brugge yenye pointi 41 nafasi ya pili.

Mtanzania huyo aliwahi kuibuka mchezaji bora wa Afrika mwaka 2015 wakati huo akiichezea TP Mazembe ya DR Congo, baada ya kuisaidia timu hiyo kuibuka na ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika msimamo wa Ligi Kuu nchini England, Cardiff wanashika nafasi ya 17 wakiwa na pointi 19 katika michezo 22 waliyocheza na sasa wanataka kujiimarisha kwa kumsajili Samatta dirisha dogo ili mzunguko wa pili wapate mabao ya kutosha.

Source : Dimba

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY