Simba waivaa AS Vita Kimafia

Simba waivaa AS Vita Kimafia

0

Simba waivaa AS Vita Kimafia

UKISIKIA umafia ndio huu, kwani wakati Simba wakitarajia kukwea pipa kesho kwenda DR Congo kuwavaa AS Vita, kuna kikosi kazi kilishatangulizwa muda mrefu kuhakikisha wanajua mbinu zote za wapinzani wao hao.

Simba wanakwenda kuwavaa AS Vita, mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, huku wakiwa na ari kubwa baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JS Saoura, mchezo uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita Uwanja wa Taifa.

Simba ndio wanaoongoza kundi L wakiwa na pointi tatu sawa na Al Ahly ya Misri, timu hizo zinapishana mabao ya kufunga na kufungwa huku AS Vita na Saoura zikiburuza mkia baada ya kupata matokeo mabaya katika michezo yao ya fungua dimba.

Kutokana na umuhimu wa mchezo huo, taarifa kutoka Simba zinadai kwamba, wameshatuma kikosi kwenda DR Congo kuweka mambo sawa ili kikosi kitakapofika kesho, kifike salama huku pia wakipewa jukumu zito la kuhakikisha wanaiba mbinu za wapinzani wao hao.

“Kikosi kinaondoka Alhamis (kesho), lakini tulishatuma wajumbe ambao kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanaweka mambo sawa. Hatutaki masihara kabisa kwani lengo letu ni kushinda viwanja vyote yani nyumbani na ugenini,” alisema kigogo mmoja wa Simba.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Wekundu hao wa Msimbazi, Patrick Aussems, alisema licha ya kuwapo katika kundi gumu lakini watapambana ili kuvuka salama na kutinga hatua ya robo fainali, huku akidai hata mchezo wao huo dhidi ya AS Vita watashambulia mwanzo mwisho ili kupata pointi tatu muhimu.

“Kawaida yangu sipendi mpira wa kujilinda mana unapoteza ladha, ndiyo maana nakwambia tunakwenda Congo kupambana ili kuondoka na pointi zote tatu ili tuzidi kujikita kileleni.

“Timu yenye washambuliaji kama Emmanuel Okwi, Meddie Kagere pamoja na John Bocco huwezi kucheza kwa kujilinda, najua utakuwa mchezo mgumu ila tumejipanga vizuri kuhakikisha tunashinda,” alisema.

Kikosi hicho cha Simba jana kiliendelea na mazoezi  katika Uwanja wa Boko Veterani kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao huo utakaochezwa Jumamosi ya wiki hii katika Jiji la Kinshasa nchini DR Congo.

Simba wameianza michuano hii hatua ya makundi kwa kishindo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JS Saoura ya Algeria na sasa wanawafuata AS Vita, huku wakiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri.

Baada ya mchezo huo, Simba watakamilisha ratiba ya mzunguko wa kwanza kwa kuwafuata Al Ahly ya Misri, mchezo unaotarajiwa kuchezwa Februari mosi mwaka huu kabla ya kuanza mzunguko wa pili na Waarabu hao, mchezo utakaochezwa Februari 12, mwaka huu katika Uwanja wa Taifa.

Simba wakimaliza mchezo huo, watakwea pipa kwenda kuwafuata JS Saoura Machi 8, mwaka huu nchini Algeria na baadaye watarudi nyumbani kumalizia kibarua chao wakiwakabili AS Vita, Machi 15, mwaka huu katika Uwanja wa Taifa.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY