Simba watoa tamko la mwisho hatma ya Okwi kwenda Kaizer

Simba watoa tamko la mwisho hatma ya Okwi kwenda Kaizer

0

BAADA ya klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kuonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, uongozi wa Wekundu wa Msimbazi hao umemweka kitimoto mchezaji huyo na kuahidi kumwongezea mkataba mpya.

Mkataba wa Okwi na Simba umebakia miezi sita kumalizika na ndio maana Kaizer Chiefs walianza kumfukuzia na inadaiwa walitenga dau la Dola za Marekani 100,000 (Sh mil 220,000).

Zahera alikuwa asaini Zambia ataja aliyemleta Yanga

Ilielezwa kuwa mshambuliaji huyo raia wa Uganda, alitakiwa kujiunga na kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini mwezi huu, lakini tayari uongozi wa Simba umekaa naye na kuzuia dili hilo.

Kutokana na mazungumzo hayo ya kuongeza mkataba mpya, inasemekana hata juzi wakati kikosi cha Simba kinaondoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, Okwi alibaki jijini kukamilisha mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya.

Inadaiwa kuwa sababu kubwa ya Okwi kubaki Simba ni kutokana na matakwa ya Kocha Mkuu, Patrick Aussems, ili aweze kusaidia katika michuano ya Ligi ya Mabingwa hasa baada ya kubaini usajili wa Walter Bwalya usingekuwa na faida.

Simba walitaka kumsajili Bwalya ili kuziba pengo la Okwi, lakini kulingana na kanuni wasingeweza kumtumia katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa kwa sababu hakuwa mchezaji anayecheza ligi ya ndani ya Tanzania.

Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba (CEO), Crescentius Magori amethibitisha kuwa wapo mbioni kumwongezea mkataba mpya mchezaji huyo

“Okwi haendi popote, bado ni mchezaji wa Simba na tunatarajia kumwongezea mkataba mpya ili kuendelea kuitumikia timu yetu, hizo habari za kuondoka hakuna klabu iliyoleta barua ya kumtaka,” alisema Magori.

Alifafanua kuwa kwa kipindi hiki hawahitaji kumwachia mchezaji ambaye anategemewa katika kikosi cha kwanza wakati wana mashindano makubwa yanawakabili.

“Tena si Okwi peke yake, wapo wachezaji wengine wanamaliza mikataba mwishoni mwa msimu huu, tunazungumza nao ili kuwaongezea mingine,” alisema Magori.

Kwa upande wake, Okwi alituambia kuwa hana mpango wa kwenda timu yoyote kwa sasa bado ataendelea kuitumikia Simba.

“Mimi bado ni mchezaji wa Simba, siwezi kwenda sehemu yoyote, nimeshaungana na wenzangu Zanzibar kujiandaa na Kombe la Mapinduzi,” alisema Okwi.

source : Bingwa

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY