Umaskini Yanga Kwisha, Bilionea ajitosa kuiokoa

Umaskini Yanga Kwisha, Bilionea ajitosa kuiokoa

0

Umaskini Yanga Kwisha, Bilionea ajitosa kuiokoa

HATIMAYE hali ngumu ya kiuchumi iliyokuwa ikiikabili Yanga kwa muda mrefu ndani ya misimu hii miwili, inaelekea tamati baada ya bilionea maarufu nchini na kwingineko kuamua kujitosa kuokoa jahazi Jangwani.

Habari kutoka ndani ya watu wa karibu na bilionea huyo asiye na makeke, zinasema kuwa baada ya uchaguzi wa Yanga unaotarajiwa kufanyika Januari 13, mwaka huu, tajiri huyo ataanza rasmi kumwaga mamilioni yake Jangwani.

Chanzo chetu hicho cha uhakika, kimetuambia kuwa tajiri huyo ambaye muda mrefu amekuwa akifanya shughuli zake nje ya Tanzania, amekuwa na mapenzi na Yanga kwa miaka mingi, japo hakuwa akiisaidia moja kwa moja.

“Anaipenda sana Yanga tangu akiwa mdogo, alikuwa akisaidia pale alipotakiwa lakini kwa siri…tangu enzi za Manji (aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga), alikuwa akitamani kuisaidia lakini alihofia mgongano wa kimasilahi ukizingatia wote ni wafanyabiashara wakubwa.

“Lakini baada ya kuona hali ni mbaya Yanga, ameamua kuingiza fedha zake kuisaidia timu iweze kusajili wachezaji wazuri, kulipa mishahara ya wachezaji hadi watendaji wengineo, kuweka kambi sehemu mbalimbali na hata kuwekeza katika miundombinu kwa maana ya uwanja, vitega uchumi na kadha wa kadha,” alisema mtoa habari wetu huyo wa uhakika.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa bilionea huyo anapima upepo kuona ni nani atashinda katika uchaguzi huo wa Yanga wa Januari 13, kwani lengo lake ni kuingiza fedha ndani ya klabu hiyo chini ya uongozi sahihi wenye mtazamo wa kimabadiliko zaidi na si vinginevyo.

“Amesema (bilionea huyo) anatamani kuona klabu ikijiendesha chini ya mfumo wa kisasa ambao utafungua milango kwa wadau mbalimbali kuwekeza badala ya kutegemea wanachama. Kila mmoja wetu anafahamu soka la kisasa linaendeshwa kwa mfumo wa kampuni na si kutegemea mtu mmoja mmoja au fedha za wanachama.

“Aliniambia kuwa ameshafanya mazungumzo na kampuni nyingi tu, zikiwamo benki kubwa na mashirika ya ndege ambao wameonyesha nia ya kuwekeza Yanga. Anakuhakikishia iwapo Yanga watampata kiongozi sahihi atakayekubalika na bilionea huyo, haitashikika kuanzia mzunguko wa pili wa Ligi Kuu (Tanzania Bara),” alisisitiza mtoa habari wetu huyo.

Alipoulizwa juu ya kiongozi ambaye bilionea huyo angetamani kufanya naye kazi, mtoa habari wetu huyo alicheka na kushindwa kumtaja jina zaidi ya kusema: “Kati ya wanaogombea, wanachama wenyewe wanafahamu ni kiongozi gani sera zake ni za mabadiliko ambaye anaamini katika kuiendesha klabu kisasa. Alishakuwa madarakani na alijaribu mfumo huu lakini hakupata ushirikiano.”

Chanzo chetu hiki kilituambia kuwa pamoja na mambo mengine, bilionea huyo amechoshwa na kitendo cha baadhi ya wajanja wanaonufaika na Yanga kuwalaghai wanachama na wapenzi wao kuwa Yusuf Manji bado ana nia ya kuisapoti klabu hiyo wakati wachezaji wakiendelea ‘kufa’ njaa.

Mtoa habari wetu huyo alionya: “Kama wanachama wa Yanga watafanya makosa kwa kumchagua mtu ambaye atabaki kuwa kivuli cha wajanja wachache kupiga pesa (fedha) na asiyekuwa na mvuto kwa matajiri wa klabu hiyo, hakika wataendelea kulialia njaa miaka nenda miaka rudi.”

Wagombea wanaowania nafasi ya mwenyekiti wa Yanga ni Dk. Jonas Tiboroha na Mbaraka Igangula ambao wote walishawahi kuwa viongozi wa Yanga kwa nyakati tofauti.

Like ukurasa wetu wa Facebook Hapa kwa habari zaidi

Wakati Igangula akiwa Makamu wa Rais wa Yanga kipindi cha uongozi wa Abbas Tarimba, Tiboroha alikuwa ni Katibu Mkuu wa klabu hiyo chini ya uenyekiti wa Manji, akiwa ndiye aliyefanikisha Simon Msuva kupata timu Morocco anakotamba hadi sasa akiitangaza vilivyo klabu yake hiyo.

Install Simba na Yanga Breaking News App

source : Bingwa

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY