Zahera : Miezi miwili tu Yanga inakuwa Tajiri

Zahera : Miezi miwili tu Yanga inakuwa Tajiri

0

Zahera : Miezi miwili tu Yanga inakuwa Tajiri

HII inaweza kuwa habari njema kwa mashabiki wa Yanga baada ya kocha mkuu wao kipenzi, Mwinyi Zahera, kutamka wazi kwamba anaweza kuifanya klabu hiyo kumaliza ukata wa kifedha ndani ya miezi miwili kutokana na hazina kubwa ya wanachama na mashabiki iliyonayo.

Yanga ni klabu kongwe nchini, lakini imekuwa ikishindwa kutumia rasilimali ilizonazo katika kujiletea maendeleo, huku baadhi ya wadau wakidai tatizo hilo linasababishwa na viongozi wanaojali masilahi yao binafsi na si ya klabu.

Pamoja na kuwa na majengo mawili katika ya Jiji la Dar es Salaam, uwanja na mamilioni ya mashabiki, bado Yanga imebaki kuwa masikini, ikilia njaa kila kukicha kiasi cha kufikia hatua ya kushindwa kulipa mishahara ya wachezaji kwa zaidi ya miezi mitatu.

Kwa kulifahamu hilo, Zahera ameamua kujitosa mzima mzima kuisaidia Yanga kujiendesha kiuchumi akiamini iwapo mambo yatakwenda kama alivyopanga, inaweza kuwa moja ya klabu tajiri Afrika.

Tayari kocha huyo ameonyesha wazi mapenzi ya dhati kwa klabu hiyo kutokana na utaratibu wake wa kuwapa posho wachezaji kila wanaposhinda mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara kama sehemu ya kuwapandisha mzuka vijana wake hao waweze kufanya vizuri zaidi.

Akizungumza na nasi jana, Zahera alisema anashangaa kuiona Yanga yenye mashabiki wengi kila kona ya nchi ikilia njaa kwani kama wakitumiwa vizuri, wanaweza kuitajirisha klabu hiyo yenye historia ya kipekee katika soka la Tanzania.

“Yanga ni klabu kubwa, lakini pia sijawahi kuona mashabiki wanapenda mpira kama hapa, watu wengi sana wanaipenda klabu hii,’’ alisema Zahera.

Alisema kutokana na wingi huo wa mashabiki, amepanga kufanya harambee kwa matawi ambapo Yanga ina matawi zaidi ya 120 Tanzania, hivyo atakachofanya ni kuzungumza nao na kuhamasisha kuchangia timu.

Zahera anasema atatumia namba maalumu kwa ajili ya matawi hayo na mashabiki kuchangia na fedha hizo kuingia moja kwa moja kwenye mfuko wa timu kama wanavyofanya kwenye taasisi nyingine.

“Nitaita matawi na mashabiki kisha tutazungumza na kutoa namba maalumu ambayo watu hao wa matawi na mashabiki wengine kuchangia,” alisema Zahera.

Katika kudhibiti mianya ya wizi, Zahera amesema atataka watu watumie namba mpya watakazotoa kwa kuwa namba zinazotumiwa sasa si za watu waaminifu.

“Sasa hivi kuna namba nyingi sana na makundi ya mitandao ya WhatsApp, lakini hakuna hesabu kamili ya fedha zinazopatikana kwa kukosa usimamizi mzuri,” aliongeza Zahera.

Mpango wake mwingine katika kuwapatia fedha wachezaji ni mashabiki kulipia pindi wanapopiga picha na wachezaji kama ilivyo kwa baadhi ya nchini za Ulaya.

“Kuna baadhi ya nchi za Ulaya shabiki hawezi kupiga picha na mchezaji bila kulipia, hivyo ili kupiga picha na mchezaji unazungumza na klabu au na mchezaji mwenyewe kisha unachangia.

“Kwa sasa kuna mashabaiki wanaweza kumpa mchezaji shilingi 10,000 hadi 15,000 ili kupiga naye picha, sasa kwanini hilo lisipitishwe kwamba shabiki anayetaka kupiga picha lazima awe na kiwango maalumu cha fedha na kama hana fedha asipewe nafasi ya kupiga picha,” aliongeza Zahera.

Like ukurasa wetu wa Facebook Hapa kwa habari zaidi

Install Simba na Yanga Breaking News App

Source : Bingwa

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY