Kenya kuchunguzwa na FIFA madai ya Kuuza mechi

Kenya kuchunguzwa na FIFA madai ya Kuuza mechi

0

Kenya kuchunguzwa na FIFA madai ya Kuuza mechi

Fifa inataka kufanyika uchunguzi kuhusiana na madai kwamba baadhi ya wachezaji wa Kenya walikabidhiwa fedha ili kuuza mechi ikiwemo mchuano mmoja wa kufuzu kwa kombe la dunia la 2010.

Hatua hiyo ya shirikisho hilo la soka duniani Fifa inafuatia uchunguzi wa awali kuhusiana na majukumu ya mchezaji wa zamani wa Kenya George Owino na Wilson Raj Perumal ambaye alihusika katika kuwarai wachezaji kuuza mechi hizo.

Ripoti ya Fifa ya kurasa 10 inasema kuwa kuna ushahidi wa wawili hao kuandaa kuendesha na kuathiri matokeo ya mechi kadhaa za kimataifa.

Madai hayo yanashirikisha mechi za kimataifa zilizochezwa na Kenya kati ya 2009 hadi 2011 ikiwemo mechi moja ya kombe la dunia dhidi ya Tunisia ambayo miamba hiyo ya Afrika Kaskazini illibuka washindi kwa 1-0.

”Bwana Owino anaonekana kuandaa, kuendesha na kuathiri na alifanya makubaliano ya kifisadi na bwana Perumal” , kulingana na uchunguzi wa awali wa Fifa.

Owino aliyeichezea Kenya kati ya 2008 na 2015 amekana madai hayo. Ripti hiyo ya mwezi Septemba 2018 imeangaziwa kwa mara ya kwanza.

Fifa inasema kuwa ilitegemea mawasiliano ya barua pepe kati ya wawili hao, kutoka mwezi Juni 2009 hadi Machi 2011, katika uchunguzi wake.

Shirikisho hilo la mjini Zurich linasisitiza kuwa Perumal , raia wa Singapore aliwasiliana na Owino na wachezaji wengine wawili katika kikosi cha Kenya wakiwa na maelekezo yanayohusiana na mechi ya mwezi Oktoba 2009 dhidi ya Tunisia.

Kulingana na ripoti hiyo ya Fifa , maelekezo hayo ya Perumal kupitia barua pepe yalisema hivi: Ujue kwamba iwapo mutapoteza 1-0 hautapata kitu. Nataka mupoteze kwa magoli 3-0.

Kuna madai zaidi kwamba Perumal alitaka mechi zisizojulikana katika michuano ya Nile basin nchini Misri mwezi Januari 2011 kuuzwa.

Mechi ya kirafiki kati ya Kenya na Afrika kusini mwezi uliofuatia pia ilichunguzwa .

Uchunguzi mwengine wa Fifa ni mpango ambao Owino alijaribu kuafikiana na Perumal ambapo raia huyo wa Kenya atasajiliwa na klabu isiojulikana nchini Australia ili kushawishi matokeo ya mechi.

”Lengo la kukupeleka huko ni kwa sababu ya kibiashara ”, Perumal aliripotiwa kuandika katika ujumbe wa barua pepe tarahe 27 mwezi Machi 2010. Lakini lazima uendelee kuwa mtiifu kwangu” .

”Mshahara wa kila mwezi utakuwa dola 30,000 za Marekani. Nataka ufanye nitakachokwambia. la sivyo hutapata mshahara wako. Tumekubaliana”.

Siku mbili baadaye jibu la Owino katika ujumbe wa barua pepe lilisema.

”Sawa hakuna tatizo kwa sababu hata mimi nataka maisha mazuri na familia yangu nitafanya unachotaka. Je kuna majaribio ama ni kazi ya moja kwa moja”.

Ushahidi wa mwisho uliowasilishwa katika ripoti hiyo ya Fifa ni ule wa barua pepe zilizotoka kwa Owino ambapo anakiri kupokea fedha kutoka kwa Perumal.

”Ndio ahsante sana na mungu akubariki”, mojawapo ya barua pepe hizo ilisema.

Perumal ambaye alikamatwa kwa kushawishi matokeo ya mechi 2011 amefichua kwamba hapo awali alifanikiwa kuingia na kushawishi mechi katika mataifa kadhaa ya Afrika.

Mara ya mwisho Owino aliichezea timu ya Kenya ya Mathare FC.

Fifa tayari inachunguza mechi nyengine ya kufuzu kwa kombe la dunia la 2010 barani Afrika kuhusiana na udanganyifu wa mechi huku ikichunguza mchuano kati ya Sierra Leone na Afrika Kusini 2008.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY