Dante Majanga

Dante Majanga

0

UKISIKIA kucheza kibingwa ndio huku mwanangu, yaani Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike inabidi apangue kikosi chake kitakachoanza dhidi ya Uganda, baada ya beki Andrew Vicent ‘Dante’ kutokuwa fiti kukiwasha kwenye mchezo huo.

Dante, ambaye amekuwa kwenye kiwango kizuri kwa sasa, anasumbuliwa na majeraha ya misuli hivyo, hatakuwa sehemu ya mchezo huo muhimu kwa Taifa Stars. Katika kikosi ambacho Amunike alikitangaza kuivaa Uganda katika kuwania kufuzu fainali za AFCON, amewaita mabeki wa kati wanne Agrey Morris, Kelvin Yondani, Andrew Vicent na Kennedy Wilson, lakini kukosekana kwa Dante kutamlizimisha kufikiri tofauti.

Lakini majeraha aliyoyapata katika mechi ya Kombe la FA dhidi ya Namungo, limemtibulia mipango yake ya kuendeleza rekodi ya kucheza kwenye kikosi hicho ikiwemo mechi za timu yake. Daktari wa Yanga, Edward Bavu alisema kuwa Dante bado hajawa fiti na hatacheza dhidi ya Uganda. “Dante hajawa fiti na nilishangaa alivyoitwa kwasababu aliumia akiwa na timu yake tukicheza na Namungo, tangu hapo alikosekana kwetu na bado ataendelea kukosekana michezo yetu ijayo,” alisema. Alisema kuwa tayari amefanya mawasiliano na madaktari wa Taifa Stars ili kuangalia namna ya kujaza pengo lake.

“Wachezaji wanatakiwa kuingia kambini sasa kama yeye akishindwa kujiunga na wenzake itakuwa kitu kingine, ndio maana nimewasiliana na wenzangu kuwapa taarifa,” alisema. Kwa upande wa Amunike alisema analipatia ufumbuzi wa haraka: “Inabidi niangalie namna itakavyokuwa muda huu ili kufanya maamuzi sahihi haraka kabla ya mchezo huo.” Stars itashuka dimbani kuikaribisha Uganda Machi 24 mchezo ambao, inapaswa ishinde ili ikate tiketi ya kucheza AFCON mwaka huu zitakazofanyika Misri.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY