Ibenge ataja wawili Simba waliomuua

Ibenge ataja wawili Simba waliomuua

0

Ibenge ataja wawili Simba waliomuua

KOCHA Mkuu wa AS Vita ya Congo, Florent Ibenge, amekiri kuwa wapinzani wao Simba walikuwa bora zaidi yao katika mchezo wa mwisho wa Ligi ya Mabingwa Afrika huku akitaja kuwa safu ya kiungo iliyochezwa na Mnyarwanda, Haruna Niyonzima na Mzambia, Clatous Chama ndiyo iliyowaletea matatizo.

Timu hizo zilivaana juzi Jumamosi katika mchezo huo uliojaa upinzani mkubwa kila timu ikijihitaji ushindi ili ifuzu hatua ya Robo Fainali ya michuano hiyo mikubwa Afrika.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Simba ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-1 kupitia kwa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Chama.

Akizungumza nasi, Ibenge alisema kuwa walikuwa na kila sababu ya kufungwa katika mchezo huo kutokana na kiwango kikubwa kilichoonyeshwa na Simba katika kipindi cha pili cha mchezo huo.

Ibenge ambaye pia ni Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya DR Congo, alisema anawatabiria Simba kufika mbali kwenye michuano hiyo kutokana na viwango vya wachezaji wake.

“Simba ilistahili kupata ushindi katika mchezo huu, kiukweli walicheza vizuri kama timu walipunguza makosa na walijituma sana, hicho ndicho kimewafanya kupata ushindi wa kufuzu Robo Fainali Afrika.

“Walijitahidi kucheza vizuri katika kipindi cha pili hasa katika safu yao ya kiungo ambayo kipindi cha kwanza iliiruhusu safu yangu ya kiungo kutawala na kufanikiwa kupata bao la kwanza.

“Kama kocha ninawatakia kila la kheri waendako na matumaini yangu kuwaona wakifanya vizuri katika hatua ya Robo Fainali ya michuano hii mikubwa,”alisema Ibenge.

Simba imefanikiwa kufuzu hatua hiyo baada ya kufikisha pointi tisa huku Al Ahly ya Misri ikiongoza Kundi D, wakiwa na pointi 10 baada ya kufanikiwa kuwafunga JS Saoura mabao 3-0.

source: Champion

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY