JPM awazawadia viwanja Stars

JPM awazawadia viwanja Stars

0

RAIS Dk. John Magufuli amewazawadia viwanja wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, baada ya kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika(Afcon 2019).

Taifa Stars ilisonga mbele baada ya kuifunga Uganda mabao 3-0 katika mchezo wa mwisho wa Kundi L uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Stars ilinufaika pia na matokeo ya mechi nyingine ya kundi hilo iliyochezwa siku hiyo, kwani iwapo Lesotho ingeifunga Cape Verde, Tanzania hata kama ingeichapa Uganda mabao 15-0, isingeenda popote.

Akizungumza katika hafla ya chakula cha mchana cha kuwapongeza wachezaji wa Stars Ikulu, Dar es Salaam jana, Dk. Magufuli alisema kuwa atakayeamua kuuza kiwanja chake sawa, japo alipendekeza waviendeleze kama kumbukumbu yao.

Mbali ya wachezaji wa kikosi hicho, pia Rais Magufuli ametoa zawadi kama hiyo kwa bondia Hassan Mwakinyo na mwakilishi wake pamoja na wanasoka wa zamani, Leodegar Tenga na Peter Tino.

Mbali ya viwanja, Rais Magufuli alimzawadia Tino Sh milioni tano kutokana na mchango wake ulioiwezesha Stars kufuzu michuano ya Afcon mwaka 1980, huku pia akiwa mmoja wa wahamasishaji wa kikosi cha timu hiyo kilichoichapa Uganda juzi, sawa na Tenga.

Rais Magufuli alisema amefurahishwa na ushindi walioupata Taifa Stars pamoja na Mwakinyo aliyemchapa Muargentina Sergio Gonzalez, Jumamosi iliyopita nchini Kenya katika pambano la Ubingwa wa Dunia (WBC) uzito wa ‘super bantam’.

Alisema viwanja hivyo vitapatikana jijini Dodoma na kumtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kushughulikia suala hilo ili kupata eneo zuri.

“Kwa wachezaji hawa wa Taifa Star kwa sababu wamenigusa, kwa niaba ya Watanzania, nawapa zawadi ndogo, hivyo wachezaji na Hassan, mwalimu wake (lakini alipewa mwakilishi wake kwa kuwa kocha wake hakuwapo Ikulu) pamoja na Peter Tino na ndugu Tenga, kila mmoja apate kiwanja chake,” alisema Rais Magufuli.

Alisema ana uhakika mapato wanayopata wachezaji hao, watumie kuendeleza viwanja hivyo ili wanapostaafu maisha yao yasiwe ya ajabu.

“Ukipata hicho kiwanja, ukiamua kukiuza shauri yako, lakini nataka sisi kama Serikali kwa niaba ya Watanzania, viwe shukurani yetu,” alisema.

Alisema kitendo cha Taifa Stars kushinda, kimefuta machungu yake yote ya nyuma yaliyosababishwa na kufungwa, ikiwamo kupoteza mechi dhidi ya Lesotho.

“Nataka niseme kwa dhati, nilikuwa nimeahidi nisiiite timu yoyote hapa Ikulu, baada ya kutandikwa kule Lesotho na mmekula milioni zangu 50, mchezo ule uliniboa kweli kwa sababu niliuangalia mwenyewe mlivyokuwa mkicheza, pasi zilizokuwa zikitolewa.

“Wachezaji wengine wazuri hawakupangwa katika nafasi zao, nikawa najiuliza huyo aliyepanga timu alipanga kwa makusudi au palikuwa na nini?

“Nakata niwaeleze ukweli, nilikuwa nimezungumza na Mwakyembe(Dk. Harrison Mwakyembe) akiwa Afrika Kusini, akaniambia timu iko safi na tunashinda, sijawahi kumpigia tena na alikuwa akiandika meseji sikumjibu hadi leo, wala sijawahi kuzungumza na Naibu Waziri (Juliana Shonza), iliniuma kweli.

“Mchezo huu matumaini ya kushinda yalikuwa hayapo kwa kuwa unaenda kucheza ukitegemea matokeo ya timu nyingine, nikaona niangalie nikiwa nyumbani kwa sababu sikutaka kwenda kupata fedheha,” alisema.

Alieleza kuwa kwa ushindi huo, vita ndiyo imeanza na endapo kikosi hicho kitaonyesha mchezo kama ilivyokuwa juzi, inaweza kufika fainali katika Afcon.

Awataka Yanga kuishangilia Simba

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliwataka mashabiki wa soka nchini kuweka pembeni itikadi za vyama na klabu zao linapokuja suala la maslahi ya taifa.

“Niwaombe vilabu (klabu) mbalimbali, hasa Simba na Yanga, inapocheza Simba kuliwakilisha Taifa, Wanayanga waishangilie, pia ikicheza Yanga, Simba waishangilie, inawezekana haya nayo ndiyo yanatuchelewesha,” alisema Rais.

Pia Rais Magufuli ameikabidhi Simba kwa Makamu wake, Samia Suluhu baada ya kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ili kuhakikisha inafanya vizuri.

Ahoji mapato ya Uwanja wa Taifa

Juu ya mapato ya uwanjani, Rais Magufuli alisema: “Unapokwenda uwanjani, ukarabati haupo vizuri, hali inayomfanya mtu kujiuliza kuwa hiyo asilimia inayokatwa inakwenda wapi.

“Katika maswali ya kawaida kama watu wengi walikatishwa tiketi, je, hazina kiwango, je, suala la ulinzi wameliangaliaje? Yapo maswali mengi ambayo yana changamoto.”

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY