Ndemla siku za kutua Yanga zinahesabika

Ndemla siku za kutua Yanga zinahesabika

0

HII inaweza isiwe taarifa nzuri kwa mashabiki wa Simba, lakini ukweli ndivyo ulivyo, kiungo wao fundi mwenye mashuti makali, Said Ndemla kwa sasa anahesabu siku tu kabla ya kuvaa uzi wa Jangwani. Ingawa imekuwa ikifanywa siri, lakini ukweli Yanga imeanza kuvuruga mipango ya Simba kwa msimu ujao, wakionyesha nia ya kumsajili kiungo Ndemla.

Ndemla amekuwa kwenye sintofahamu baada ya dili lake ya Sweden alikokwenda kufanya majaribio mara mbili kwenye klabu ya AFC Eskilstuna na hadi sasa hakuna kinachoendelea.

Imeeleezwa vigogo wa Yanga mapema wiki hii walikutana kuzungumzia ishu ya kumsajili Ndemla msimu ujao wa Ligi Kuu na kama watafikia makubaliano basi huenda akatimkia Jangwani.

Mazungumzo hayo yamedaiwa kufanyika kwa usiri mkubwa kwani mchezaji huyo bado ana mkataba na Simba ingawa pia inadaiwa mkataba huo unamalizika mwishoni mwa msimu huu. Chanzo kutoka ndani ya Yanga, kinaeleza mazungumzo ya pande hizo mbili yanakwenda vizuri.

Maamuzi hayo yamedaiwa ni kutokana na kwamba, nyota huyo hapati nafasi kubwa ya kucheza ndani ya kikosi cha Kocha Patrick Aussems raia wa Ubelgiji huku wengi wakiamini ubora wa kiungo huyo.

“Ni kweli kuna mazungumzo yaliyofanywa dhidi ya Ndemla ila tunapaswa kusubiri mwisho utakuwaje,” kilisema chanzo hicho.

Mwanaspoti linafahamu kwamba Ndemla alisaini mkataba mpya na Simba baada ya ya viongozi wake kuvutana kwa muda mrefu wakati huo ana mpango wakutimkia Sweeden huku pia akihusishwa kujiunga na Yanga.

Mwanasheria wa mchezaji huyo, Eric Kelvin aliliambia Mwanaspoti kuwa; “Kila kitu kuhusu Ndemla kitawekwa wazi hapo baadaye mara baada ya mambo yote kuwa sawa, ila kwasasa inabaki kuwa siri kati yangu na mteja wangu.”

Uongozi wa Simba umesema hautakuwa na pingamizi endapo mchezaji huyo atapata timu nyingine kwani wanachojali pia ni kulinda kiwango cha wachezaji wao kwa kucheza.

Source : Mwanaspoti

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY