Niyonzima : Nilicheza nikiwa majeruhi

Niyonzima : Nilicheza nikiwa majeruhi

0

LICHA ya kucheza kwa kiwango kikubwa katika mechi ya AS Vita, kiungo wa Simba, Haruna Niyonzima amebainisha kwamba kwenye mechi hiyo alikuwa akicheza huku akiwa majeruhi.

Niyonzima, raia wa Rwanda, amekuwa gumzo kubwa baada ya kucheza kwa kiwango cha juu wakati klabu yake ilipokuwa inapambana na AS Vita katika Ligi ya Mabingwa, wiki iliyopita.

Mnyarwanda huyo aliingia katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Taifa Dar, dakika ya 57 akichukua nafasi ya Emmanuel Okwi na kuchangia upatikanaji wa bao la pili la Simba. Simba ilishinda kwa mabao 2-1.

Niyonzima ameeleza licha ya kuonyesha uwezo mkubwa mbele ya Wacongo hao lakini alijitonesha jeraha lake la enka ikiwa ni muda mfupi baada ya kuingia akitokea benchi lakini akaendelea kucheza bila ya kutaka kufanyiwa mabadiliko. “Machi 16, 2019 ilikuwa siku kubwa kwangu katika klabu yangu.

Ninamshukuru kocha kwa kuweka imani kwangu, lakini dakika chache nikiwa uwanjani nilihisi maumivu mabaya juu ya mguu wangu (enka). “Nilijiambia mwenyewe jambo hilo haliwezi kunifanya nikatolewa nje kwani nimefanya kazi kwa bidii kwenye mazoezi kwa jambo muhimu kama hili.

“Hii ilikuwa ni ndoto yangu tangu nikiwa mtoto kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa hivyo hakuna chochote kitanizuia na kushindwa. Kwa hivyo nilijiambia nitapambana kwa moyo wangu, sikuhitaji kucheza na mwili wakati moyo wangu ulikuwa na nguvu,” alisema Niyonzima

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY