Serengeti Boys kwenda Qatar

Serengeti Boys kwenda Qatar

0

TIMU ya soka ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, Serengeti Boys, inatarajia kuondoka kesho kwenda Qatar kuweka kambi ya wiki moja kujiandaa na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), zitakazoanza Aprili 14 hadi 28, mwaka huu hapa nchini.

Akizungumza nasi jana, kocha msaidizi wa timu hiyo, Maalim Saleh, alisema maandalizi ya kikosi hicho yamekamilika na wachezaji wapo fiti kushiriki fainali hizo kikamilifu.

Alisema wakiwa nchini Qatar watafanya mazoezi na kucheza mechi za kirafiki na wenyeji wao pamoja na timu nyingine kutoka mataifa ya karibu.

Aidha, kocha huyo alisisitiza kuwa kikosi hicho kinahitaji kufanya maandalizi ya kutosha hasa baada ya hivi karibuni kushindwa kutamba katika michuano iliyofanyika nchini Uturuki.

Aliongeza kuwa wakiwa Qatar watayafanyia kazi makosa yaliyojitokeza wakati wanashiriki michuano ya nchini  Uturuki iliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwa kushirikiana na lile la Ulaya.

“Kinachohitajika ni kuwanoa vijana huku tukirekebisha makosa yaliyoonekana katika mechi zilizopita, tulijifunza mengi tulipokuwa Antalya, lakini kubwa zaidi morali ya wachezaji ipo juu na wana kiu ya kufanya vizuri,” alisema Saleh.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY