Tetesi za usajili Yanga Leo 24 April 2019

Tetesi za usajili Yanga Leo 24 April 2019

0

HATIMAYE Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amehakikishiwa kusajili wachezaji sita wa nguvu wa kimataifa watakaokifanya kikosi chake kuwa tishio katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Msimu huu haukuwa mzuri kwa timu hiyo kutokana na kushindwa kusajili wachezaji wa kiwango cha juu, hali iliyosababisha mashabiki wao wasiwe na matumaini ya kutwaa ubingwa na hata kufanya vizuri kimataifa.

Hata hivyo, mara baada ya msimu kuanza kikosi cha Zahera kilifanya vizuri katika mechi za mwanzo na kujikuta kikiongoza ligi kwa muda mrefu kabla ya kupoteza mwelekeo kwenye mechi za hivi karibuni walipokubali vipigo ama kutoa sare.

Japo Yanga inaongoza ligi kwa sasa ikiwa imekusanya pointi 74, lakini matumaini ya kutwaa ubingwa yanaonekana kufifia.

Hilo linatokana na ukweli kwamba Simba waliocheza mechi chache wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa iwapo watashinda mechi zao 10 zijazo, kwani watakuwa wamewapita pointi wapinzani wao hao.

Kwa kufahamu hilo, mabosi, matajiri wa Yanga na mashabiki, wameamua kujipanga upya kwa ajili ya msimu ujao wakipania kusajili wachezaji wa kiwango cha juu hasa kutoka nje ya Tanzania.

Tayari kocha wa Wanajangwani hao, Zahera, ameweka wazi kitita cha fedha  anazohitaji ili kumwezesha kusajili wachezaji anaowataka kikosini.

Katika mahojiano na BINGWA, Zahera alisema anahitaji kitita cha Dola za Marekani 300,000 (sawa na Sh milioni 689) kusajili wachezaji watakaokuwa tishio na kumaliza kabisa ubabe wa wapinzani wake.

“Nina imani katika kiasi hicho siwezi kukosa wachezaji kumi wa Dola za Marekani 30,000 (sawa na Sh milioni 70) ambao wataifanya Yanga kuwa tishio msimu ujao,” alisema Zahera.

Kutokana na ombi hilo la Zahera, Mwenyekiti wa Yanga bungeni, Anthony Mavunde, amesema kwamba tayari wameshapata fedha za kuwawezesha kusajili wachezaji zaidi ya sita wenye kiwango cha kimataifa.

Alisema fedha hizo walizozipata kupitia michango ya wabunge na wadau wengine nchini, zinaweza kuongezeka na hivyo kusajili wachezaji wengi zaidi wenye kiwango cha juu.

“Tunawaomba wote wanaoitakia mema Yanga wajitokeze kuichangia timu yao ili uongozi mpya utakapopatikana uweze kushirikiana na mwalimu wetu Zahera kusajili wachezaji watakaoifanya Yanga kuwa moto msimu ujao,” alisema Mavunde.

Hadi sasa Wanajangwani hao wamecheza michezo 32 na kujikusanyia pointi 73, wakishinda 23, sare tano na kufungwa nne.

Katika michuano ya kimataifa iliyopita, Yanga ilishindwa kufanya vizuri na hata michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika tofauti na watani wao wa jadi Simba waliofika hadi hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Sababu kubwa zilizoibeba Simba msimu huu ni kikosi chao kusheheni wachezaji wenye kiwango cha juu na uzoefu kama Meddie Kagere, Erasto Nyoni, Clatous Chama na wengineo.

Source : Bingwa

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY