Usajili: Watatu toka Simba wanatua Yanga

Usajili: Watatu toka Simba wanatua Yanga

0

Yanga imepokea majina mawili, wa kwanza ni winga ambaye wanaona hatumiwi vizuri na Simba, Mghana Nicholas Gyan ambaye hatma yake sasa itakuwa kwa kocha Mwinyi Zahera.

Ndoa ya Gyan na Simba yaani ligi ikimalizika tu nayo inakuwa imemaliza uhai lakini pia wekundu hao wakipiga hesabu za kumtema baada ya kuona hafai wao wakimtumia kama beki wa kulia na Yanga wanaona jamaa hawajui matumizi sahihi ya straika huyo wa zamani wa Ebusua Dwarfs ya Ghana.

Gyan mwenyewe inaelezwa amewaambia Yanga kuwa hana tatizo lakini pia anaona anakosewa kutumiwa kama beki kitu ambacho kimewasukuma mabosi wa Yanga kumjadili zaidi. Kiasili Gyan ni straika na wakati mwingine hucheza kama kiungo mshambuliaji wa pembeni.

JUUKO NDANI

Mbali na Gyan staa mwingine ni beki kisiki Juuko Murshid raia wa Uganda ambaye naye jina lake limo ndani ya simu za mabosi wa Yanga wakimjadili kwa mapana na marefu.

Juuko mkataba wake naye unaisha mwisho wa ligi huku Simba nao wakiona beki huyo anakuwa hatari anapovaa jezi ya taifa lake lakini anaporudi kwao hawamwelewi ingawa kuna muda wanasita kumuacha.

“Tunaangalia kipi kifanyike hatutaki kufanya uamuzi wa papara kama ni mchezaji tunataka kuangalia uwezo wake wa kufanya kazi hilo ndiyo tunataka kulifanya sasa sio usajili wa kishabiki huo hapa kwetu hatuna kwasasa,” alisema mmoja wa vigogo wa Yanga (aliyeombwa kuhifadhiwa jina).

Kigogo huyo alidokeza kuwa, kwa sasa hatma ya wawili hao ipo kwa Zahera katika kikao kijacho ambacho atafanya na mabosi wa Yanga ambapo atasogezewa majina hayo kisha kutoa majibu ya wasajiliwe au vinginevyo.

NDEMLA NAYE YUMO

Kama hiyo haitoshi ni kwamba Kiungo Said Ndemla taarifa ni kwamba ameshafanya vikao kadhaa na mabosi wa Yanga na kinachosubiriwa ni hatma ya viungo watatu wa nje ambao Yanga inawawinda kwa usiri mkubwa.

Yanga wanataka kujua hatma ya viungo hao kama watakubali kutua klabuni kwao na kama itawapata wawili katika hao basi itaachana na Ndemla, lakini kama mambo yatakuwa magumu usajili wa kiungo huyo mwenye mashuti itakuwa ni kazi rahisi kumnasa.

Ndemla alihusishwa kutua Yanga kwenye dirisha dogo kabla ya mabosi wa Simba kuamua kumpa mkataba chapchapu licha ya ukweli hatumiki sana kwenye kikosi cha Patrick Aussems, ingawa ni wao Simba waliokiibuka kipaji chake kupitia timu yao ya Vijana U20 miaka michache iliyopita.

Yanga ni kama imekuwa na hasira na Simba hasa baada ya kusikia wameshamalizana na Ajibu waliyemchukua kutoka kwao msimu uliopita.

Source : Mwanaspoti

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY