Ajibu atembea na mkataba wa Yanga

Ajibu atembea na mkataba wa Yanga

0

UONGOZI mpya wa Yanga chini ya Mwenyekiti wake, Mshindo Msolla umeanza mazungumzo na wachezaji wake muhimu nyota wanaomaliza mikataba yao.

Baadhi ya wachezaji ambao mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu ni Ibrahim Ajibu anayeelezwa kusaini mkataba wa awali (Pre Contract) Simba, Pappy Tshishimbi, Haji Mwinyi, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe na Mrisho Ngassa.

Yanga imepanga kukisuka kikosi chake chini ya kocha mkuu wa timu hiyo, Mkongomani, Mwinyi Zahera ili kuhakikisha wanachukua makombe yote yatakayoyashindania kwenye msimu ujao.

Taarifa ambazo Championi Jumatano inazo ni kwamba katika kikao kilichowakutanisha kamati ya utendaji ya timu hiyo hivi karibuni, wameweka mikakati thabiti ya kuhakikisha wanawabakisha wachezaji wote ambao kocha amependekeza wabakishwe.

Mtoa taarifa huyo alisema, viongozi wameanza kufanya mazungumzo na wachezaji aliowapendekeza ili kabla ya ligi kumalizika wawe washamalizana nao.

Aliongeza kuwa, kamati hiyo ya utendaji imepanga kutoruhusu mchezaji anayehitajika na kocha kuondoka.

“Hatutakuwa tayari kumuachia mchezaji yeyote tutakayemuhitaji kati ya hao wanaomaliza mikataba yao, hiyo yote katika kukiimarisha kikosi chetu kwa msimu ujao.

“Na hilo linawezekana kwetu na tayari tumeshaanza kufanya mazungumzo na wachezaji wetu na lengo ni kuirejesha Yanga anga za kimataifa, lazima tuwe na kikosi kipana kitakacholeta changamoto ya ushindani wa kitaifa na kimataifa.

“Tumepata taarifa za baadhi ya wachezaji wetu kufanya mazungumzo na wengine kusaini mkataba wa awali timu nyingine, sisi kama uongozi hatuliangalii hilo na zaidi tutafanya mazungumzo na kila mchezaji atakayekuwa kwenye mipango ya kocha wetu,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa Zahera kuzungumzia hilo alisema: “Tayari nina orodha ya wachezaji wapya ninaotaka kuwasajili kwa ajili ya msimu ujao na kati yao yupo mshambuliaji kutoka Gabon, winga na beki mmoja wa kati wote raia wa DR Congo.

“Pia, nina majina ya wachezaji niliyoyapendekeza kwa ajili ya kuwaacha kwa wale wasiocheza nusu ya mechi za msimu huu ambao wanajijua na tayari nimeshakabidhi majina yao.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY