Dante: Wachezaji Yanga ni vidume

Dante: Wachezaji Yanga ni vidume

0

BEKI wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’, amesema licha ya kukosa ubingwa msimu huu, lakini wachezaji wa kikosi hicho wanastahili pongezi nyingi kutokana na uvumilivu walioonyesha.

Akizungumza na BINGWA jana, Dante, alisema hawajawahi kupitia kipindi kigumu kama ilivyo msimu huu, lakini wachezaji walionekana kuendelea kuipambania timu hadi muda huu wanamaliza katika nafasi ya pili.

Dante alisema wachezaji wa Yanga wamekuwa na uvumilivu wa kipekee, isingekuwa rahisi kwa timu nyingine kustahimili matatizo waliyopitia ukizingatia huko nyuma walishazoea kuishi vizuri.

“Kwa msimu huu kitu ambacho sitasahau ni changamoto tulizopitia, lakini bado tulikuwa tunapambana na dalili za kuchukua ubingwa zilikuwepo, ila  mwishoni ikawatofauti kutokana na matokeo ya mpira.

“Hakuna asiyejua Yanga tumepita kipindi kigumu kiasi gani, tulikuwa tunaishi tu na hata uongozi haukuwepo, lakini leo hii tunamaliza nafasi ya pili sio mbaya, kazi kubwa tumeifanya na kilichochangia ni uvumilivu wa wachezaji,” alisema Dante.

Alieleza kuwa kutokana na hali hiyo, kikosi hicho kinastahili kuwekwa miongoni mwa timu bora  na wachezaji  wamekuwa mfano wa kuigwa kwa  kuonyesha uvumilivu, huku wakipigania  timu yao.

“Malengo yetu ilikuwa kuchukua ubingwa bila kujali hali yetu na ndiyo sababu tulikuwa tunapambana kila  sehemu, lakini bahati haikuwa yetu na tunashukuru  hata kwa hapa tulipofikia kwa kumaliza nafasi ya pili,” alisema.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY