Hizi ndizo mashine za kimataifa zilizotua Yanga

Hizi ndizo mashine za kimataifa zilizotua Yanga

0

YANGA wamepania aisee. Unaambiwa saa chache baada ya kuhakikisha kiungo fundi, Papy Kabamba Tshishimbi amesaini mkataba wa miaka miwili, Kocha Mwinyi Zahera ameonyesha hatanii kwani ule mpango wake wa kukijenga kikosi kibabe umeanza.


Ndio, juzi Ijumaa si Mkongo huyo alipokea mashine nne matata ambazo jana Jumamosi zilikuwa zikifanya majaribio na kikosi cha sasa cha Yanga, lakini habari zikufike kuwa, jana alfajiri Mkongo huyo ameshusha beki mkali akiipokonya klabu yake ya zamani.


Zahera amemleta nchini beki Mghana, Lamine Moro akitokea klabu ya Buildcon ya Zambia ambayo ameifanyia umafia mzito.


Zahera mara ya kwanza alikutana na Lamine wakiwa klabu hiyo ambayo ilikuwa inakaribia kumpa mkataba kocha huyo Mkongomani kabla ya Yanga kubadili upepo na kumsomba kocha huyo.


Katika kusuka safu ya ulinzi, Zahera amemvuta beki huyo mrefu na anayetumia kimo chake vyema kukabiliana na mipira ya juu.
Ujio wa beki huyo ulikuwa wa kificho kikubwa kutokana na Lamine kuwahi kuhitajiwa na Simba kabla ya Wekundu hao wa Msimbazi hawajabadili upepo wakimtaka kurudi baadaye kutokana na kutokuwa na uwezekano wa kumsajili katika dirisha la usajili lililopita.


Juzi alfajiri, Lamine alitua rasmi Yanga na leo yumo ndani ya moja ya hoteli za jiji la Dar es Salaam akisubiri kumalizana na Kamati ya Usajili ya Yanga iliyo chini ya Mwenyekiti wake, Frank Kamugisha.

Kwa Tetesi za Usajili kila siku Install App yetu


Akizungumza baada ya kuwasili, Lamine alisema amekuja kuungana na kocha wake huyo (Zahera) ambaye alikuwa akimhitaji kwa muda mrefu aliyemzuia kusaini katika klabu nyingi zilizokuwa zikimtaka kumsajili.


“Nimekuja kuungana na kocha wangu Zahera, amekuwa akiwasiliana nami kwa kipindi kirefu na ilikuwa niwe nimejiunga na klabu nyingine, lakini nimeona nije kuungana na kocha Zahera,” alisema Lamine aliyewahi kufanya mazoezi na kuichezea Simba katika mechi za michuano ya SportPesa Super Cup 2019 kabla ya Msimbazi kumpotezea.


Akizungumzia uwezo wake, alisema Zahera anaujua vyema na ndio maana amemuita nchini, lakini pia Wanayanga wataona makali yake mara baada ya kumalizana na klabu hiyo.


“Kocha anaujua vyema uwezo wangu ndio maana nipo hapa, lakini mashabiki wa Yanga wataona uwezo wangu nitakapoanza kazi,” alisema Lamine.


Mbali na beki huyo, pia zipo mashine nyingine nne ambazo jana zilikuwa zikipiga tizi na nyota wengine wa Yanga kwa ajili ya majaribio.
Nyota hao wanne waliotua Yanga ni Wanigeria, Victor Patrick Akpan na Shehu Magaji Bulama; Mguinea, Mohammed Ali Camara na Alex Komenan ambaye ni raia wa Ivory Coast.

Mwanaspoti

Kwa Tetesi za Usajili kila siku Install App yetu

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY