Mashine ya Singida Hiyooo Jangwani

Mashine ya Singida Hiyooo Jangwani

0

MKATA umeme wa Singida United, Kenny Ally amesema yuko tayari sasa kuitumikia Yanga msimu ujao kwani tayari mabosi wake wa Singida wameshampa mkono wa kwa heri ili ajiunge na mabingwa hao wa kihistoria Tanzania.

Kenny alijiunga na Singida United misimu miwili iliyopita na kuisaidia timu hiyo kucheza fainali za Kombe la Shirikisho la Azam, ambapo mkataba wake wa kuitumikia umefikia ukingoni huku Yangawakiwa tayari kumsajili msimu ujao.

Akizungumza nasi, Kenny Ally alisema kuwa, tayari Singida wamempatia mkono wa kwa heri, hivyo msimu ujao hana shaka yoyote tena ya kuitumikia Yanga, zaidi anasubiria ligi imalizike aweze kusaini Yanga.

“Nipo tayari sasa kuitumikia Yanga baada ya kunihitaji kwa muda mrefu, huku nikishindwa kuungana nao kutokana na kuwa na mkataba na Singida ambao ulinibana, kwa sasa nipo huru kuichezea kwani Singida wameridhia hilo,” alisema Ally.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga yeye amesema wao hawana shida juu ya hilo.  “Sisi hatuna tena kipingamizi na Kenny Ally kwani tayari tumeshamalizana naye hivyo lililobaki ni jukumu la wao Yanga kukaa naye mezani na kuelewana namna watakavyompatia maslahi yake tu.

“Tulimsajili kwa gharama kubwa ambayo kwa sasa akiihitaji hatuna tena uwezo huo wa kumpatia, hivyo tunatoa baraka zote za kwenda Yanga, maana wameonyesha nia ya muda mrefu kuhitaji huduma yake,” alisema Sanga.

Ikumbukwe kuwa Yanga imekuwa ikimuwinda kiungo huyo aliyewahi kuitumikia Mbeya City tangu wakati wa usajili wa mwanzoni mwa msimu huu.

Champion

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY