Yanga ya Karne

Yanga ya Karne

0

MAMBO yamezidi kunoga Yanga kuhusiana na suala zima la usajili, ambapo uongozi wa klabu hiyo umesisitiza kutotaka masikhara katika mchakato huo, mkakati wao ukiwa ni kunasa wachezaji watakaounda kikosi cha karne.

Achana na kufanya vibaya msimu uliopita na kujikuta wakipoteza ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara au mwenendo wao wa sasa unaotishia kuwatoa kappa.

Kilichowapandisha hasira watu wa Yanga na kujikuta wakipigia hesabu wachezaji wa kiwango cha kimataifa ni kitendo cha watani wao wa jadi, Simba, kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba walifika hatua hiyo kutokana na kuwa na kikosi kipana kilichohusisha wachezaji wa kiwango cha juu na wenye uzoefu kama wazawa Erasto Nyoni, Jonas Mkude na John Bocco, lakini pia nyota wa kigeni Clatous Chama (Zambia), Emmanuel Okwi na Jjuuko Murushid (Uganda).

Wengine ni Meddie Kagere na Haruna Niyonzima (Rwanda), James Kotei, Nicholas Gyan na Asante Kwasi (Ghana), Zana Coulibaly na Pascal Wawa (Ivory Coast).

Kwa kiasi kikubwa, wakali hao hapo juu pamoja na kipa wao, Aishi Manula, ndio walioiwezesha Simba kuwa tishio kwa vigogo wa soka Afrika kama Al Ahly ya Misri, TP Mazembe na AS Vita za DR Congo, Nkana ya Zambia na nyinginezo zilizokutana na Wekundu wa Msimbazi hao.

Ni kutokana na kufahamu hilo, Yanga wamepania kujibu mapigo ili kukata ngebe za mashabiki wa Simba ambao wamekuwa wakiwabeza mno msimu huu wakidai kikosi cha Wanajangwani hao ni cha ‘mchangani’ hakina uwezo wa kufua dafu kimataifa.

Na sasa wakati wakiwa na kitita cha nguvu kinachotajwa kufikia Sh bilioni mbili zilizopatikana kupitia harambee ya kuichangia, Yanga ina uhakika wa kusajili wachezaji 10 watakaoifanya timu yao kuwa tishio hapa nchini na Afrika kwa ujumla.

Tayari Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera raia wa DR Congo, amepanda ndege kwenda kumalizana na wachezaji aliowasiliana nao katika nchi mbili Afrika, japo amekataa katakata kuyataja mataifa hayo kwa hofu ya kuhujumiwa.

Akizungumza na BINGWA jana, Zahera alisema: “Nipo katika Uwanja wa Ndege wa Addis Ababa (Ethiopia), naenda kukutana na wachezaji ninaowataka, nitarejea Tanzania Mei 18 (mwaka huu).

“Wachezaji hao ninawaangalia kwenye nchi mbili za Kiafrika ambazo siwezi kuzitaja.”

Wakati Zahera akiwa angani kuwafuata nyota hao anaowahitaji kwa udi na uvumba, uongozi wa Yanga jana ulifanya mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu yao yaliyopo makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga, Dar es Salaam na kuweka wazi mikakati yao katika suala zima la usajili.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Yanga, Dk. Mshindo Msolla, alisema kuwa wiki ijayo watakutana na Zahera ili kutaja orodha ya wachezaji aliowapendekeza.

Msolla alisema kuhusu suala la usajili mipango yote wamemwachia kocha huyo, kuhakikisha anatafuta wachezaji bora anaowahitaji kwa kiasi chochote cha fedha kitapatikana.

“Mchakato wa usajili unaendelea, wiki ijayo tutakutana na kocha ili kupata orodha ya wachezaji anaowahitaji, kila kitu tumemwachia yeye, sisi atatuletea tu kuwa nahitaji hiki,” alisema Msolla.

Hata hivyo, alisema katika kupata kikosi kipana zaidi, wamewapa kazi wachezaji wa zamani wa Yanga kwenda mikoani kusaka vipaji kuungana na wale atakaoleta kocha.

Miongoni mwa wachezaji wa zamani wa Yanga wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo ni Sunday Manara, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, Edibily Lunyamila na wengine wengi.

“Pia tunatarajia kuunda Kamati ya Usajili itakayofanya kazi pamoja na benchi la ufundi katika kuweka sawa na mipango ya kupata kikosi kinachohitajika,” alisema Msolla.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamasishaji na Uchangiaji Yanga, Lucas Mashauri, alisema wadau wa klabu hiyo wanaendelea kuchangia na kiasi cha fedha wanachohitaji kitapatikana.

“Zahera tumempa uhuru hata akitaka mchezaji kutoka Ulaya sisi tupo tayari kutoa fedha hizo, kwa sababu bajeti ni shilingi bilioni 1.5 hadi bilioni mbili,” alisema Mashauri.

Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 83 baada ya kucheza mechi 36, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 82, lakini ikiwa imeshuka dimbani mara 33 tu, ikibakiza michezo mitano dhidi ya miwili ya watani wao hao wa jadi.

Pamoja na kuongoza ligi hiyo, bado nafasi ya Yanga kutwaa ubingwa ni finyu kwani Simba wana michezo mingi mkononi hivyo wanaweza kuzipita pointi walizonazo watani wao hao wa jadi na kubeba ‘mwali’ iwapo watashinda yote.

Bingwa

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY