Maajabu makubwa yaliyotokea Ligi kuu TPL

Maajabu makubwa yaliyotokea Ligi kuu TPL

0

.Wakati Ligi Kuu Tanzania Bara imemalizika maajabu 10 yalisisimua mashindano hayo yaliyoshirikisha timu 20 ambapo Simba ilitwaa ubingwa kwa mara ya pili mfululizo.


Maajabu hayo 10 bila shaka yanaweza kutokea katika ligi ya Tanzania licha ya kuwa na wigo mpana katika sekta ya michezo nchini.
Pamoja na matukio hayo yasiyotarajiwa katika mchezo wa soka duniani, Simba ilipewa kombe lake katika mechi ya mwisho waliyotoka suluhu na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.


Pia timu mbili za African Lyon na Stand United ziliteremka daraja wakati Kagera Sugar na Mwadui ya Shinyanga ambazo zitacheza na timu za Daraja la Kwanza Pamba na Geita.


Viporo
Moja ya maajabu ya ligi hiyo msimu huu ni pamoja na mechi za viporo ambazo zilitia fora kwa klabu ya Simba ambayo ilikuwa nyuma kwa zaidi ya michezo 11.
Simba iliyokuwa ikishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ilikuwa na mechi 11 mkononi za viporo ikiwa imebakiza raundi tatu kabla ya kumalizika.
Simba iliyotupwa nje katika robo fainali ilikuwa imecheza mechi 22 tu, wakati baadhi ya timu kama Mbao FC, African Lyon, JKT Tanzania, Stand United na Singida United zikuwa zimecheza michezo 33.


Yanga, Azam


Wakati Simba ikiwa haijacheza mchezo wowote na timu nne huku ligi ikiwa katika mzunguko wa pili, Yanga ilikuwa haijavaana na Azam katika mechi zote mbili za mzunguko wa kwanza na pili.
Timu hizo zilivaana katika mechi za ‘jioni’ za mzunguko wa pili ambapo mchezo wa kwanza Yanga ilishinda bao 1-0 kabla ya Azam kulipa kisasi kwa kuilaza mabao 2-0 katika mchezo wa kufunga pazia la Ligi Kuu.


Mashabiki


Tukio jingine ambalo halikuwa la kawaida katika ligi hiyo msimu huu ni lile la Jumamosi Aprili 6 katika mchezo baina ya Prisons na Biashara United ambapo zilipatikana Sh9,000 kama mapato ya mlangoni.
Ni mashabiki watatu tu ndio waliokata tiketi kushuhudia mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya ambapo kiingilio kilikuwa Sh3,000.


Gari la Wagonjwa
Tatizo la ukosefu wa gari la wagonjwa viwanjani lilikuwa changamoto katika ligi hiyo na mfano wake ni mechi ya Mbao dhidi ya Coastal Union katika mechi ya mzunguko wa kwanza.
Pamoja na matukio hayo kujitokeza mara kwa mara kwenye viwanja tofauti, lakini lile la beki wa Coastal Adeyum Seleh alilazimika kupelekwa hospitali kwa kutumia gari binafsi aina ya Harrier kumpeleka hospitali kwa matibabu.


Mdhamini
Kitendo cha Ligi Kuu kuchezwa bila mdhamini mkuu, kilichangia kwa kiasi kikubwa mashindano hayo kukosa mvuto kama ilivyotarajiwa kutokana na ukubwa wake.
Idadi kubwa ya timu zilicheza katika mazingira magumu baada ya ligi kukosa mdhamini na baadhi ya viongozi walilazimika kutoa fedha zao za mfukoni kuokoa jahazi.


Mipira
Maajabu mengine ambayo yametokea msimu kutokuwa na mdhamini kumefanya kutokuwepo na vifaa vya kutumika kama mipira ambayo ilikuwa ikitolewa na kampuni ya mawasiliano ambayo ilikuwa ikitoa mipira, jezi na viatu.
Msimu huu Simba katika mechi zao zote ilitumia mipira yake katika kucheza na hata katika moja ya mchezo ambao ilicheza mkoani ilipoteza mpira mmoja ambao mpaka wanamaliza ziara yake ya kucheza michezo mitatu katika ukanda wa mkoa huo hawakurudi nao.
Katika mechi za Simba dhidi ya Yanga na Azam timu hizo katika mipira 10 ambayo ilikuwa ikitumika ilikuwa ikitoa mipira mitano ili kuchezewa katika mchezo husika.


Kagera Sugar, Stand United
Sintofahamu na taharuki iliyodumu kwa saa 19 baada ya msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2018-2019 kumalizika, ilihitimishwa, baada ya Bodi ya Ligi (TPLB) kutangaza rasmi kushuka daraja timu ya Stand United badala ya Kagera Sugar.
Saa chache baada ya ligi kumalizika kuliibuka sintofahamu kuhusu timu ipi kati ya hizo mbili inatakiwa kushuka daraja kulingana na kanuni na msimamo wa ligi ulivyokuwa baada ya kumalizika.


Taharuki hiyo iliibuka baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa msimamo wa ligi ulioonyesha Kagera Sugar imemaliza ikiwa nafasi ya 19 na hivyo kulazimika kuungana na African Lyon iliyotangulia mapema kushuka daraja na Stand United iko nafasi ya 18 ambayo inailazimu kucheza mechi za mchujo dhidi ya timu ya Pamba ya Ligi Daraja la Kwanza.
Msimamo huo uliotolewa na TFF ulionyesha timu zote zimemaliza zikiwa na idadi sawa ya pointi 44, zina uwiano sawa wa mabao ya kufunga na kufungwa -11, hivyo Stand United inakaa juu ya Kagera Sugar katika msimamo wa ligi kwa kunufaika na kigezo cha tatu kwenye kanuni ya kumpata mshindi pindi timu zinapolingana pointi ambacho ni idadi ya mabao ya kufunga.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY