Tetesi za usajili Simba Leo 9 June 2019

Tetesi za usajili Simba Leo 9 June 2019

0

KIMYA kingi kina mshindo. Hivyo ndivyo inavyotarajiwa kuwa ndani ya Simba kwani viongozi wa klabu hiyo, wanatarajiwa kuwashtua wapenzi wao kwa kuwashushia wachezaji wenye viwango vya juu, wakifanya hivyo kimya kimya.

Mbali ya nyota kadhaa wa ndani wanaotajwa, wakiwamo Ibrahim Ajib aliyemaliza mkataba Yanga, pia Simba inatajwa kumweka kati mshambuliaji wa zamani wa Azam, Shaaban Chilunda aliyekuwa akicheza soka la kulipwa nchini Hispania katika kikosi cha Tenerife.

Habari kutoka kwa watu wa karibu na Chilunda, zinadai kuwa nyota huyo wa timu ya Taifa, Taifa Stars, alikuwa katika mazungumzo na viongozi wa Simba muda mfupi kabla ya kikosi cha Emmnuel Amunike kupanda ndege kwenda Misri kuweka kambi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon2019) itakayofanyika nchini humo.

“Jamaa (Chilunda) ni msiri sana, nina wasi wasi alikutana na watu wa Simba na usishangae kuja kusikia amesaini mkataba nao kabla ya kuondoka na kikosi cha Taifa Stars kwenda Misri,” alisema mtoa habari wetu huyo.

BINGWA liliwatafuta viongozi wa Simba kuzungumzia juu ya hilo na usajili wao kwa ujumla, lakini wengi waliopigiwa simu, walikataa kutoa ushirikiano.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescetius Magori, alisema: “Usajili bado, tunamalizana na wachezaji wetu wa ndani kwanza, kila kitu kitafahamika mara baada ya kumalizana na hawa.”

Lakini habari kutoka kwa kiongozi wa klabu hiyo ambaye hakupenda jina lake kuwekwa wazi, zinasema kuwa Mwenyekiti wao wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji ‘Mo’, amesisitiza kutokubali kuona mtu yeyote akiwapelekea mchezaji wa ‘kuungaunga’.

“Mo hataki utani kabisa katika suala la usajili, amesema mtu yeyote atakayempelekea mchezaji, basi awe ni mchezaji kweli na si wa kubahatisha. Anataka wachezaji wenye viwango zaidi ya akina Chama (Clatous), Kagere (Meddie) au Okwi (Emmanuel).

“Ndio maana husikii kuna mtu amemleta mchezaji kirahisi kama msimu uliopita ambao wengine walichukua muda hadi kuchanganya na kupata namba, hilo halipo kabisa safari hii,” alisema.

Alisema hata kambi ya timu hiyo kujiandaa na msimu ujao, inatarajiwa kuwa ‘bab kubwa’, ikiwekwa katika nchi iliyo juu kisoka, zaidi ikitajwa Ufaransa, japo awali zilihusishwa nchi kama Uturuki na hata Marekani na Ureno.

“Awali ilikuwa ni Marekani au Ureno, baadaye ikatajwa Uturuki. Lakini habari za hivi karibuni, nasikia kambi inaweza kwenda kuwekwa Ufaransa,” alisema kiongozi huyo akiomba kuhifadhiwa.

Msimu uliopita, Simba ilifanya vizuri mno katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufika robo fainali, lakini pia ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mafanikio hayo yalitokana na usajili wa nguvu uliofanywa na viongozi wa klabu hiyo, wakiwamo Kagere, Chama, Okwi, Pascal Wawa, James Kotei na wengineo.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY